Kuhusu Takwimu za Asasi za Kiraia Zanzibar

Historia fupi / Utangulizi

Takwimu hii ni juhudi ya Wizara ya Katiba na Utawala Bora - Zanzibar ambayo ndiyo yenye dhamana ya kusajili na kuratibu shughuli za Asasi za Kiraia. Kituo cha kulelea Asasi Zisizokuwa za Kiserikali( NGO Resource Centre) ambacho ni Mradi wa Aga Khan Foundation; kimesaidia sana kiutaalamu katika kufanikisha kazi hii kwa kutumia CD - ROM na nakala zilizochapishwa. Kazi hii ya Takwimu inakusudiwa kuwa ni Kituo Kikuu cha Habari za Asasi za Kiraia ziliopo Zanzibar.

Katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 sasa kumekuwa na mfumuko/ongezeko la wa Asasi mbalimbali za Kiraia zisizofungamana na lengo la kupata madaraka ya kisiasa au faida za Kibiashara. Asasi hizi zimejikita katika maswala ya maendeleo ya kijamii; zimo zile za Kamati za Vijiji, za Kidini, za Kikabila, za Kikazi, Kitaalamu na nyenginezo.

Serikali ya Zanzibar inathamini na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Asasi za Kiraia katika kutatua matatizo ya Kijamii ikiwemo kupambana na Umaskini. Vilevile katika kuthamini mchango huo; Asasi za Kiraia zimepewa majukumu makubwa katika Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) katika juhudi za kusaidia kupambana na Umasikini Kitaifa.

Kuhusu Takwimu Hii

Utengenezaji wa Takwimu hii ulipitia hatua tatu kuu; Hatua ya kwanza muhimu ilihusisha kupata orodha ya Asasi za Kiraia ziliopo Ofisi ya Msajili Mkuu, Wizara ya Katiba na Utawala Bora.Kwa kutumia Orodha hii tulijaribu kuzithibitisha baadhi ya Asasi ziliopo. Hatua ya Pili ilitumia utaratibu wa Dodoso ambazo Wizara ilizigawa kwa Asasi ambazo zimejisajili Serikalini; kuthibitisha na kurekebisha Taarifa zao za awali. Matangazo kwa njia ya Televisheni na Redio yalitolewa kuelezea madhumuni ya zoezi hilo na kutaja vituo vya kukusanyia Dodoso hizo zilizojazwa. Hatua ya tatu na ya mwisho ilikuwa ni kuthibitisha maelezo yaliyomo kwenye Dodoso hizo. Mara tu Asasi hizo ziliporejeshwa Dodoso hizo ilichaguliwa nusu ya sampuli ya Asasi zote zilizosajiliwa kuthibitisha uhai wao kama maelezo yao yalivyojazwa katika fomu.Tunawahakikishia wengine kwamba Asasi zote 226 ambazo zimejikita katika kujaza na kutuma Dodoso zao zipo kiuhakika.

Marekebisho ya Takwimu

Takwimu hii ya 2007 ya Asasi za Kiraia Zanzibar haihusishi Asasi zote za Kiraia zinazofanya kazi hapa Zanzibar.Takwimu hii imehusisha zaidi Asasi za Kiraia zilizoitikia mwito wa kujaza habari zao katika kipindi maalum na habari hizo kuthibitishwa na field team.Tunatoa wito kwa Asasi za Kiraia ambazo hazikuwasilisha fomu zao zilizojazwa katika wakati uliotakiwa kuharakisha zoezi hilo ili taarifa zao ziweze kuingizwa kwenye Takwimu hii.Wito huu unahusisha Asasi mpya na ziliopo.

Tanbihi

Ingawaje kila tahadhari imechukuliwa kuingiza habari za uhakika kama zilivyotolewa na Asasi husika lakini si Wizara wala NGO Resource Centre itakayobeba jukumu la taarifa zenye makosa zinazotokana na Asasi hizo. Asasi zilizoorodheshwa kwenye Takwimu hii zinaomba kuchukua nafasi ya kurekebisha taarifa walizozitoa ambazo zinamakosa hasa katika tafsiri ambayo itakuwa inabadilisha maana. Kwa kiasi kikubwa tunaamini kwamba hii ni rikodi ya uhakika wa Asasi za Kiraia zinazofanya kazi Zanzibar kuanzia mwishoni mwa 2007.